Ssamexa.blogsport.com
Kirusi
cha utoro ambacho kimekuwa kikilitesa Bunge la Muungano wa Tanzania kwa
muda mrefu, sasa kimeingia kwa kishindo kwenye Baraza la Wawakilishi
(BLW), ambako shughuli za baraza hilo zimekuwa zikikwama kutokana na
wajumbe kutohudhuria vikao. Hali hiyo ilijitokeza tena tangu wakati wa
kikao cha kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15 kilichoanza Mei 14,
mwaka huu na kumalizika wiki iliyopi.
Tatizo
hilo la utoro wa wawakilishi wa wananchi hapa nchini awali lilidhaniwa
kwamba ni la Bunge la Muungano pekee, ambako chombo hicho kwa miaka
nenda miaka rudi kimekuwa kikikaa na kupitisha bajeti za Serikali na
kufanya uamuzi katika mambo nyeti ya taifa pasipo kuwapo akidi, kinyume
cha Katiba na Kanuni za Bunge. Udhaifu huo umekuwa tatizo sugu, kwani
hata Bunge la Bajeti lililokaa mjini Dodoma kuanzia mwanzoni mwa Mei
kujadili Bajeti ya mwaka 2014/15 lilimalizika wiki iliyopita likiwa
limepitisha baadhi ya mambo nyeti pasipo kuwapo akidi.
Pamoja na
utoro wa wabunge kwenye Bunge la Muungano kuwa tatizo sugu kiasi cha
wananchi na wabunge wenyewe kuliona la kawaida, limekuwa halipigiwi
kelele hata pale picha za magazeti na televisheni zinapoonyesha viti
vingi bungeni vikiwa vitupu wakati vikao vya maamuzi muhimu vikiendelea.
Tatizo hapa ni kukosekana vifungu katika Katiba au Kanuni za Bunge za
kuwapa wananchi madaraka ya kuwawajibisha wawakilishi wao kwa kuwapigia
kura ya kutokuwa na imani nao.
Hata
hivyo, haikutazamiwa kwamba Baraza la Wawakilishi nalo lingekumbwa na
tatizo hilo, kwani lilikuwa na mwenendo mzuri wa uwajibikaji baada ya
kuanzishwa mwaka 1984 na kuendelea hivyo hadi mfumo wa Serikali ya Umoja
wa Kitaifa (SUK) ulipoanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Inasikitisha kwamba utoro sasa umeanza kuwa tatizo kubwa kwenye Baraza
hilo, hata kuwaweka katika hali ngumu Spika Pandu Ameir Kificho, naibu
wake, Ali Abdallah Ali na mwenyekiti wa Baraza hilo, Mgeni Hassan Juma
kiasi cha chombo hicho kushindwa kukaa kama Kamati ya Matumizi kutokana
na kutotimia akidi ya asilimia 50.
Katika
tukio la wiki iliyopita, Naibu Spika Ali Abdallah Ali aliahirisha Baraza
hilo kutokana na uchache wa wajumbe wakati wa kujadili bajeti ya Wizara
ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati iliyowasilishwa na Waziri Ramadhan
Abdallah Shaaban. Hivyo, Baraza hilo lisingeweza kukaa kama Kamati ya
Matumizi na kupitisha vifungu kutokana na akidi ya wajumbe kutofikia
asilimia 50. Tukio hilo lilitanguliwa na lile la Baraza hilo kushindwa
kukaa kama Kamati ya Matumizi chini ya mwenyekiti wake, Mgeni Hassan
Juma wakati wa kujadili bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko.
Hiyo ni mbali na matukio mawili ya awali, wakati Spika Kificho
alipoliahirisha kwa sababu ya kukosekana akidi.
Tungependa
kutoa hadhari kwa wajumbe wote wa BLW kwamba vitendo vyao vya utoro
siyo tu ni utovu wa nidhamu, bali pia vinahatarisha uhai wao katika
Baraza hilo.
Tofauti
na wapigakura wa Tanzania Bara, wenzao wa Zanzibar ni makini mno katika
kufuatilia uwajibikaji wa wawakilishi wao, kwani historia imeonyesha
kuwa, pamoja na kutokubali kuhongwa, hawana simile wala huruma na
wawakilishi wanaowasaliti kwa kutotimiza wajibu wao.
CHANZO:MWANANACHI
No comments:
Post a Comment