samexa.blogsport.com Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene
MAJERUHI
wa bomu lililolipuliwa katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine
jijini Arusha juzi, wanachunguzwa na Jeshi la Polisi na Idara ya
Uhamiaji.
Taarifa
za awali ambazo gazeti hili lilizipata jana, zilidai tukio hilo la bomu
linatokana ugomvi wa kibiashara. Taarifa hizo zilidai kuwa Jeshi la
Polisi lilikuwa linaendesha uchunguzi wa tukio hilo na pamoja na madai
kuwa linatokana na ugomvi wa kibiashara.(Martha Magessa)
Alipohojiwa
kwa njia ya simu jana juu ya tukio hilo na madai kuwa kuna hisia
linatokana na ugomvi wa kibiashara, Mkurugenzi wa Idara ya Habari
(MAELEZO), Assah Mwambene alisema, “ni kweli na mimi nimesikia taarifa
hizo, lakini tuviachie vyombo vya ulinzi na usalama, vilifanyie kazi
tukio hilo na vitatoa taarifa kamili vikimaliza uchunguzi wao”.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Daniel
Namomba, alisema jana ofisi yake inafanya uchunguzi kuhusu majeruhi wa
tukio hilo, kubaini kama uwepo wao nchini ulikuwa ni wa kihalali.
Namomba
alisema wanapitia nyaraka zote za majeruhi hao ili kujua kama wapo,
waliokuwa wanafanya kazi hapa nchini kwa vibali maalumu; na endapo
kulikuwa na watalii kati yao, ambao waliingia nchini kihalali.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi jana, ofisa huyo alisema, “Siwezi
kuthibitisha kama majeruhi hao walikuwa hapa nchini kihalali au la,
naomba unipe muda kwa kuwa suala hili ofisi yangu inalifanyia kazi na
baada ya uchunguzi kukamilika nitatoa taarifa rasmi”.
Kumekuwepo
taarifa jijini hapa kwamba mfanyabiashara mwenye asili ya Asia (jina
tunalo), ndiye aliyekuwa mwenyeji wa majeruhi hao, wanaodaiwa kuwa
watalii, huku taarifa nyingine zikidai ni wafanyabiashara wa madini.
“Majeruhi
hawa wapo ambao ni wafanyakazi hapa (Arusha) kwa zaidi ya miaka 15,
lakini baadhi yao siyo raia na inadaiwa kuwa ni watalii na wengine
wanadai walikuja hapa zaidi ya wiki moja iliyopita kwa lengo la kufanya
biashara ya madini,” alisema mmoja wa watu, ambaye hakutaka jina lake
litajwe gazetini.
Waziri hospitalini
Katika
hatua nyingine, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Seif Rashid
alitembelea majeruhi jana katika Hospitali ya Rufaa ya Seliani.
Waziri
huyo alilaani vikali kitendo hicho kilichofanywa na watu ambao
wanahatarisha amani ya jiji la Arusha, ambalo ni kitovu cha utalii
nchini.
Alisema
hali za majeruhi zinaendelea vizuri. Alisisitiza kwamba vyombo vya
ulinzi na usalama, vinaendelea na uchunguzi kubaini watuhumiwa hao
hatimaye wafikishwe kwenye mkono wa sheria.
Matibabu Nairobi
Waziri
alisema endapo wagonjwa watasafirishwa nje ya nchi, serikali haitahusika
katika matibabu yao, kwa kuwa anaamini nchini kuna hospitali zenye
uwezo mkubwa wa kutibu majeruhi.
Akizungumzia
hali za majeruhi hao, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Seliani, Dk Mark
Jacobson ambaye ni raia wa Marekani, alisema hali za wagonjwa
zinaendelea vizuri.
Lakini,
alisema mmoja kati ya wagonjwa hao, ambaye ni mtoto wa miaka (13),
Ritwik Khaalelwa, amepelekwa Nairobi kwa matibabu kutokana na hali yake
kutoridhisha.
Aidha,
alisema Deeptak Gupta aliyepoteza mguu wa kushoto, bado yuko katika
chumba cha uangalizi maalumu, kutokana na maumivu makali aliyo nayo na
familia yake inafanya utaratibu wa kumhamishia Nairobi kwa matibau
zaidi.
Jacobson
alisema wagonjwa wengine wawili wanaendelea na matibabu hospitalini
hapo. Alisema watatu wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya majeraha
waliyoyapata, kuendelea vizuri.
Mbatia ahofu
Mwenyekiti
wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia ametaka Serikali kupitia Idara
yake ya Ulinzi na Usalama wa Taifa, kurudi kazini na kufanya uchunguzi
wa kina juu ya milipuko ya mabomu, yanayotokea Jijini Arusha na kutoa
majibu sahihi ya matukio hayo.
Mbatia, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema hayo jana jijini hapa, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema
mashambulio hayo katika jiji la Arusha lenye vivuto vingi vya utalii,
yanatisha na yanasikitisha na uchumi wa nchi unaweza kuyumba kwa matukio
hayo.
Mbatia
alisema Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vya utalii
vingi na uchumi wa nchi katika sekta ya utalii, pato lake ni sawa na
asilimia 17 sawa na Sh trilioni 9.6 kwa mwaka.
Alisema
watu na mali zao katika maeneo ya Jiji la Arusha na Zanzibar, wanapaswa
kulindwa kwa nguvu zote.Alisema serikali inapaswa kufuatilia na kutambua
adui wanayepambana naye.
Alishauri
serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kukusanya kila
kiashiria cha matukio hayo bila kudharau na kisha kukaa mezani kwa
kushirikisha watu mbalimbali, kuchambua kwa kina kila kimoja kupata
ukweli na kisha kuufanyia kazi.
Viashiria
Alitaja
baadhi ya viashiria vilivyowahi kutajwa na makundi mbalimbali kuwa ni
ugomvi wa kisiasa, dini, wivu wa kibiashara ya utalii na kusherehekea na
kushabikia matukio ya uvunjifu wa amani katika nchi jirani.
Vingine
ni ugomvi wa marais na mgogoro wa kutaka kumng’oa Spika wa Bunge la
Afrika Mashariki. Alisema utaratibu wa sasa wa serikali na vyombo vya
usalama, kutoa majibu mepesi kila tukio linapotokea, bila kutoa majawabu
sahihi, ni dalili za kushindwa kutafutia ufumbuzi matukio hayo, hali
inayoendelea kujenga hofu miongoni mwa wananchi.
Alionya
kuwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, haipaswi kusubiri hadi
jambo litokee, ndipo ianze kupambana bali inapaswa kujipanga,
ikizingatiwa tukio hilo la jana si la kwanza, bali ni la sita ndani ya
kipindi cha mwaka na nusu.
Mbatia
alisema alitegemea muda huu angeona anga la Arusha likiwa limefunikwa na
helikopta na pia kukiwa na askari wa kutuliza ghasia mitaani.
Alisema
kwa mkoa wa Arusha kuendelea kukumbwa na matukio hayo ya mabomu,
kunaathiri mambo mengi, ikiwemo pato la taifa, ikizingatiwa utalii
unachangia asilimia 33 ya pato la taifa.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment