Thursday 10 July 2014

FILIKUNJOMBE KUWALIPUA BUNGENI MAKANDARASI WABOVU LUDEWA , ASIFIA KAMPUNI YA BOIMANDA

Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe kushoto akishirikiana na mwananchi wa Lupingu kukata mti uliokuwepo katika njia ya kupitisha umeme kutoka Ludewa kwenda Lupingu baada ya mbunge huyo kushinda siku nzima akishiriki maendeleo ya kupeleka umeme Lupingu jumla ya vijiji 49 Ludewa kupelekewa umeme

Mbunge Filikunjombe wa pili kulia akimsikiliza mwakilishi wa meneja wa Tanroads mkoa wa Njombe Bw KIndole wakati akielezea maendeleo ya ujenzi wa barabara Ludewa 
MBUNGE wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe amepania kutumia dakika zake 15 bungeni kuwalipua makandarasi wabovu wanaoendelea na ujenzi wa barabara mbali mbali katika wilaya ya Ludewa ikiwemo barabara ya Njombe -Ludewa na Ludewa - Manda(Martha Magessa)
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo juzi wakati akikagua ujenzi wa barabara hizo katika wilaya ya Njombe na kuwa katika baadhi ya maeneo hajafurahishwa na utendaji kazi wa kampuni husika kutokana na kufanya kazi hiyo chini ya kiwango na kuwa hadi sasa ni kampuni moja pekee ambayo imeonyesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa .
" Serikali imewekeza mabilioni ya shilingi katika ujenzi huu wa barabara katika wilaya ya Ludewa na lengo likiwa ni kusaidia wananchi kuondokana na adha ya ubovu wa barabara .....sasa nikiwa kama mbunge mwakilishi wa wananchi nitakuwa mtu wa mwisho kufumbia macho uchakachuaji mkubwa unaofanywa na baadhi ya makandarasi hao"
Alisema hadi sasa ni kampuni moja pekee ya Boimanda ambayo imeonyesha uzalendo wa kweli katika ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe katika wilaya ya Ludewa ila makampuni yaliyosalia yamekuwa yakifanya uchakachuaji mkubwa katika ujenzi huo na kuwa zaidi ya makampuni manne ndio yanahusika na ujenzi huo kwa kila kampuni kupewa kipande.
Hivyo alisema mara baada ya kurejea bungeni kwa kikao kijacho cha bunge moja kati ya mambo ambayo atafikisha bungeni ni pamoja na shukrani kwa kampuni ya Boimanda inayoongozwa na mkurugenzi wake Nicholaus Mgaya kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa wa kazi ila pia kufikisha kilio chake dhidi ya makandarasi wabovu wanaoendelea na ujenzi huo.
Filikunjombe alisema kasoro ambazo amepata kuziona kwa makandarasi hao ni pamoja na kujenga barabara bila kuweka mifereji ya kupita maji ,kudanganya ujazo wa kifusi kinachopaswa kumwagwa barabarani pamoja na mlazo mzuri wa barabara baada ya kuchongwa .
Kwani alisema iwapo kasoro hizo hazifanyiwa kazi basi ni wazi barabara hizo hazitadumu na baada ya mvua kunyesha ni wazi Ludewa itarejea katika kero yake ya mwanzo ya ubovu wa miundo mbinu.
Pia alisema kwa mujibu wa mikataba makandarasi hao wanapaswa kukabidhi barabara hizo tarehe 23 mwezi huu ila ukitazama ukubwa wa kazi iliyobaki ni wazi kutakuwepo na ubabaishaji mkubwa katika kumalizia kazi hiyo kwa ubora.
Wakati huo huo mbunge huyo amempongeza Rais Dr Jakaya Kikwete kwa kutekeleza ahadi yake kwa wana Ludewa juu ya uboreshaji wa barabara hizo kwa lengo la kuwezesha wawekezaji wa madini ya liganga na Nchuchuma kufanikisha kupitisha mitambo yao .
Alisema kuwa uwajibikaji wa serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Dr Kikwete imekuwa ikileta matumaini makubwa kwa watanzania hasa wananchi wa jimbo la Ludewa ambao kwa muda mrefu sasa hawajapata kuwa na barabara za lami .
Aidha alimpongeza waziri wa ujenzi Dr John Magufuli kwa kuendelea kuwa waziri wa mfano katika baraza la mawaziri nchini kutokana na usimamizi mzuri wa miradi ya barabara japo alisema wanaoendelea kumuangusha ni makandarasi wasio wazalendo.
CHANZO:Francis Godwin

Tuma Maoni..0718192930 samexavery@yahoo.com//samexa.blogsport.com

No comments:

Post a Comment