Tuesday 8 July 2014

BRAZIL 2014: NI NOMA: Brazil v Ujerumani na Uholanzi v Argentina ni kama fainali

Mechi zote ni kama fainali. Brazil itamalizana na Ujerumani leo Jumanne kwenye Uwanja wa Estadio Mineirao wakati Uholanzi na Argentina zamu yao ni kesho Jumatano uwanjani Arena de Sao Paulo.
Kila mechi mmoja lazima afe. Ni watu wachache wanaoweza kutabiri mechi hizi kumtambua nani atatinga fainali itakayopigwa Jumapili uwanjani Maracana jijini Rio de Janeiro.
Takwimu zinaonyesha kwamba timu za Amerika Kusini zitashinda. Lakini, vigogo vya Ulaya vilivyotinga hatua hiyo, Uholanzi na Ujerumani, vyote vipo makini na vinacheza soka la maana. Timu nne zilizobaki zote ni bora.
Hata hivyo hakuna timu ya Ulaya iliyowahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia lililofanyika Amerika. Mara saba ya fainali hizo zilipofanyika kwenye bara hilo, kombe limebaki huko. Brazil ilinyakua mara tatu, Argentina na Uruguay kila moja ilibeba mara mbili.
Presha imempanda kocha wa Ujerumani, Joachim Low na kusema: “Timu za Amerika Kusini zina faida ya kucheza nyumbani. Hilo halina ubishi. Wanafahamu mazingira yao na wanaweza kuyatumia.”
Ujerumani itawavaa Brazil, mabingwa mara tano wa fainali hizo na pia ni wenyeji. Ujerumani inakumbuka ilivyochapwa na Brazil kwenye Kombe la Dunia mwaka 2002 lililofanyika Korea Kusini na Japan.
Kipindi hicho kwenye benchi la Brazil kulikuwa na kocha Luiz Felipe Scolari kama ilivyo sasa.
Lakini, kikosi cha Brazil kitakosa huduma ya mastaa wake wawili makini, Neymar aliyevunjika mfupa wa mgongo na nahodha wao, Thiago Silva, anayetumikia adhabu ya kadi.
Kwenye timu hizo nne zilizotinga nusu fainali ni Uholanzi pekee ambayo haijawahi kuwa bingwa. Lakini, iliwahi kukaribia kuutwaa ubingwa mara tatu. Safari hii wanaonekana kuwa wapo vizuri zaidi chini ya kocha Louis van Gaal. Dhidi yao na Argentina patachimbika.
Kila mmoja ana nafasi yake. Historia itabadilika au itabaki kama ilivyo? Tusubiri.

No comments:

Post a Comment